Luka 12:4-7 - 16-09-2026

Date
Reading
Luka 12:4-7

Jumatano asubuhi 16.09.2026;

Luka 12:4-7

4 Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi.

5 Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo.

6 Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu.

7 Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

Mungu hujishughulisha na mambo yetu;
Asubuhi hii tunamsoma Yesu akifundisha juu ya kumkiri bila woga. Anawafundisha mkutano kwamba wasiwaogope wauao mwili tu, bali wamwogope yule awezaye kumwua mtu na kumtupa Jehanam. Kwenye Injili ya Mathayo anaeleza vizuri, kwamba mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.

Mathayo 10:28

Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.

Yesu anaendelea kuonesha umuhimu wa waliomsikiliza katika safari ya imani. Anatoa mfano wa mashomoro ambao walikuwa ndege waliouzwa kwa bei ndogo, lakini hakutakiwa kuanguka hata mmoja. Sasa Yesu anawaambia wasikilizaji wake kwamba wao ni muhimu kuliko mashomoro wengi, hivyo wasiogope. Yesu anatupa ujasiri wa kumfuata siku zote za maisha yetu, hivyo tumwamini yeye ajishughulishaye na mambo yetu. Amina

Siku njema

Heri Buberwa