Mwanzo 12:10-20 - 18-09-2026

Date
Reading
Mwanzo 12:10-20

Ijumaa asubuhi tarehe 18.09.2026;

Mwanzo 12:10-20

10 Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.

11 Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso;

12 basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai.

13 Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.

14 Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana.

15 Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao.

16 Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia.

17 Lakini Bwana akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu.

18 Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo?

19 Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako.

20 Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho. 

Mungu hujishughulisha na mambo yetu;

Njaa ilikuwa kubwa katika nchi, Abramu (baadaye Abraham) akaenda Misri kujinusuru na njaa. Sarai (baadaye Sara) alikuwa mwanamke mzuri, hivyo akamwambia aseme ni ndugu yake, maana ingejulikana ni mke wake wangemuua. Walipofika Misri Farao akamtwaa Sarai, lakini Mungu akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu kwa ajili ya Sarai aliyekuwa amemtwaa. Baada ya kupigwa na Bwana, Farao akamwachia Sarai.
Tunaona Mungu akijishughulisha na Abramu kwa;
1. Kumuepusha na njaa kwa kumuongoza kuelekea Misri
2. Kumfanya Sarai mkewe asitwaliwe katika nchi ya ugeni
Nasi tuzidi kumtegemea Kristo ambaye hujishughulisha na mambo yetu. Amina

Siku njema

Heri Buberwa