
Jumanne asubuhi tarehe 27.10.2026;
Habakuki 2:18-20
18 Sanamu ya kuchora yafaa nini, hata yeye aliyeifanya ameichora? Sanamu ya kuyeyuka, nayo ni mwalimu wa uongo, yafaa nini, hata yeye aliyeifanya aiwekee tumaini lake, na kufanya sanamu zisizoweza kusema?
19 Ole wake yeye auambiaye mti, Amka; aliambiaye jiwe lisiloweza kusema, Ondoka! Je! Kitu hicho kitafundisha? Tazama, kimefunikwa kwa dhahabu na fedha, wala hamna pumzi ndani yake kabisa.
20 Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake.
Mwenye haki ataishi kwa imani;
Somo la asubuhi ya leo ni unabii unaotofautisha ibada ya sanamu na ukuu wa Mungu. Pamoja na kuchongwa vizuri, kupambwa na kurembwa, sanamu inabaki ni sanamu tu. Nabii Habakuki anawaonya watu kwa kuamini miungu badala ya Mungu. Anahitimisha kwa kuwataka wamwabudu Mungu wa kweli akisema "Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake"
Mtume Paulo alimnukuu Habakuki alipoandika kwamba mwenye haki ataishi kwa imani;
Habakuki 2:3-4
3 Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.
4 Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.
Kwa hiyo Habakuki anapowazuia watu kufanya ibada ya sanamu, anawataka kumwabudu Mungu wa kweli. Anawataka kuwa na imani ya kweli katika Bwana. Ndiyo wito tunaopewa asubuhi ya leo, kumwamini Yesu Kristo aliye njia ya kweli na uzima. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
