Jumatatu asubuhi tarehe 13.07.2026
1 Samweli 20:35-42
35 Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye.
36 Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake.
37 Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako?
38 Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake.
39 Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe.
40 Naye Yonathani akampa mtoto silaha zake, akamwambia, Nenda, ukazichukue mjini.
41 Basi mara alipokuwa amekwisha ondoka yule mtoto, mara Daudi akatoka mahali pale karibu na kile kichuguu, akaanguka kifudifudi, akajiinama mara tatu; nao wakabusiana, wakaliliana, hata Daudi akazidi.
42 Naye Yonathani akamwambia Daudi, Enenda kwa amani; kwa maana sisi sote wawili tumeapiana kwa jina la Bwana ya kwamba, Bwana atakuwa kati ya mimi na wewe, na kati ya uzao wangu na uzao wako milele. Daudi akaondoka, akaenda zake; Yonathani naye akaenda zake mjini.
Upendo wa Mungu na utawale;
Sura ya 20 ya kitabu cha kwanza cha Samweli inahusu urafiki wa kweli uliokuwepo kati ya Daudi na Yonathani, maana Yonathani alimsaidia Daudi kumuepuka Sauli aliyetaka kumuua. Mstari wa 42 unaonesha urafiki wa dhati kati ya Daudi na Yonathani (soma mstari wa 42 tena kwenye somo hapo juu). Inaonekana nguvu ya urafiki, umuhimu wa kuaminiana na kuisikia sauti ya Mungu wakati wote zikiwemo nyakati za hatari.
Urafiki wa Daudi na Yonathani ulikuwa wa wazi, kujitoa, na kusaidiana katika hali zote. Waliapiana kwa jina la Bwana kuwa Bwana angekuwa kati yao, na hata kati ya uzao wao. Huu ulikuwa ni urafiki mkubwa sana, wa kuiga. Yaani urafiki wao uliwekwa katika Bwana. Kumbe na sisi tupendane katika Bwana, yaani upendo wa Mungu utawale miongoni mwetu. Amina
Uwe na wiki njema yenye upendo.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
