
Jumatatu asubuhi tarehe 21.09.2026;
Yohana 9:35-41
35 Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?
36 Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?
37 Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye.
38 Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.
39 Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.
40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?
41 Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.
Mungu amejaa huruma;
Yesu alikuwa amemponya mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Mafarisayo walihoji uponyaji huo, maana hawakumuamini Yesu, halafu ulifanyika siku ya sabato! Somo linaonesha Yesu akiongea na aliyeponywa na kumsisitiza amwamini Yesu aliye Mwana wa Mungu. Mafarisayo walijiona wanaona lakini kwa kutokuamini kwao Yesu aliwaambia kuwa walikuwa vipofu.
Uponyaji wa Yesu kwa kipofu ni upendo na huruma yake. Yesu anaonesha kuwa amekuja duniani ili wote wapate kuona, yaani waokolewe. Anatuita asubuhi ya leo akitukumbusha kukaa kwake na kumtegemea katika yote maana yeye ndiye mwenye huruma. Tuikimbilie huruma ya Mungu ili tuwe na mwisho mwema. Amina
Uwe na wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio
Heri Buberwa
