Jumapili tarehe 12.07.2026;
Siku ya Bwana ya 6 baada ya Utatu;
Masomo;
Zab 73:22-28
1 Yoh 3:17-20
*Yer 31:1-3
Yeremia 31:1-3
1 Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.
2 Bwana asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.
3 Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.
Upendo wa Mungu na utawale;
Utangulizi;
Somo la leo ni upendo wa Mungu kwa watu, unaoonekana kwa Mungu kuwaahidi watu wake kuwatoa uhamishoni Babeli. Ili kuweka somo vizuri, tuanzie nyuma kidogo, yaani sura ya 30. Katika sura ya 30, linaonekana Taifa lililokuwa kwenye dhiki kubwa. Katika dhiki hiyo, Bwana anasema atawaokoa kutoka katioa hali hiyo ya dhiki na shida. Israeli wanapewa uhakika wa katika nchi yao, nchi ambayo baba zao walipewa na Bwana. Mstari wa 9 unaonesha ahadi yao kumtumikia Bwana, na Daudi mfalme wao ambaye Mungu angemwinua siku hiyo.
Hapa muhimu kukumbuka kwamba Daudi alikuwa amekuwa mfalme miaka zaidi ya mia nne iliyopita wakati wa unabii huu wa Yeremia. Lakini ujumbe huu ulimaanisha Kristo ajaye. Katika Yeremia 23:5 tunasoma kwamba zipo siku zinakuja ambazo Bwana angemchipushia Daudi chipukizi la haki, na siku zile Yuda angeokolewa, na Israeli kukaa salama. Kwa hiyo Yeremia anapomtaja Daudi katika kuwaokoa Israeli kutoka uhamishoni, anamtabiri Yesu atakayekuja kuokoa ulimwengu. Hitimisho la sura ya 30 hakika ya Israeli kuwa watu wa Mungu, na yeye kuwa Mungu wao, akiwaondolea hasira yake. Angalia anavyomaliza;
Yeremia 30:22-24
22 Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
23 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea tufani ya kudumu; itawaangukia waovu vichwani.
24 Hasira kali ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kutenda, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtayafahamu haya.
Somo lenyewe;
Baada ya ahadi ya Taifa la Mungu kuokolewa na kurudi katika nchi waliyopewa Baba zao kama tulivyoisoma sura ya 30, sura ya 31 ni Bwana akionesha upendo wake usiokoma kwa Taifa lake.
Mstari wa 1 ni ahadi ya Bwana kuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao kuwa watu wake. Jambo la muhimu hapa ni upendo anaouonesha Mungu kwa jamaa "zote" za Israeli. Mungu haoneshi kubagua. Ahadi yake ni kwa wote. Kumbe upendo wa Mungu kwa watu wote haujaanza leo, ni wa zamani zote na milele yote. Mfano mdogo, ndiyo maana Kanisani anaingia mtu yeyote kwa sababu Mungu habagui yeyote, anatuita wote. Wajibu wetu kuamini tu, na kuamini ni bure.
Mstari wa 2 unasomeka "Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani...." Hapa Bwana alikuwa anawakumbusha Israeli wakati walipokuwa jangwani wakaiona neema yake. Aliwatunza jangwani wasiangamie. Ni rejea ya jinsi Mungu alivyowatunza wakitoka Sinai (Hes 10:33) Katika historia ya Israeli yote na kushindwa kwao, Mungu aliendelea kuwa mwaminifu kwao akiwapenda, yaani aliendelea kudumisha ahadi ya upendo wake kwao. Kwa rejea hiyo walikuwa wanapewa ahadi ya kutoka uhamishoni. Upendo wa Mungu siku zote umekuwa wa kuwaleta watu kwake.
Mstari wa 3; Yeremia anasisitiza Bwana kuwatokea watu wake tangu kale akiwapenda, tena kwa ahadi ya upendo wa milele. Ahadi ya upendo walikuwa wanapewa ili wasiogope, wawe na hakika ya kurudi kwao. Mungu aliendelea kutoa ahadi hii;
Malaki 1:2
Nimewapenda ninyi, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Umetupendaje? Je! Esau siye ndugu yake Yakobo? Asema Bwana; ila nimempenda Yakobo;
Ni ahadi iliyoendelea kudumu, ambayo katika Agano jipya Yohana anaishuhudia wazi kwa mstari wake maarufu;
Yohana 3:16
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
--Hapa tuamini kwamba upendo wa Mungu kwetu ni wa kale, leo na siku zote.
Upendo wa Mungu na utawale;
Tumeona upendo wa Mungu kwa watu wake, akiwapa ahadi ya kurejea katika nchi yao ambayo walirejea kwa shangwe. Ujumbe mkuu katika somo ni Upendo wa Mungu kwa watu wake, kama tulivyoona akitoa uhakika wa jamaa zote za Israeli kuwa watu wake. Ahadi hiyo ipo kwetu hata sasa, maana kwa upendo wake ametuokoa bure. Kwa njia ya ubatizo tumeokolewa sote. Wapo baadhi wanaojiona wameokoka kuliko wengine, ni waongo, wabinafsi, hawana upendo kama wa Kristo. Yeye anao upendo kwetu sote, ndiyo maana kwa njia ya ubatizo ametupokea sote, anatutunza hadi mwisho wetu na kutupa uzima wa milele pale tunapoishi kwa njia ya neno lake na kumcha.
Kama Kristo alivyotupenda, nasi tupendane kwa mfano huohuo. Tusijidanganye, huwezi kumpenda Mungu kama humpendi jirani yako unayemuona. Huko ni kujifariji, ni uongo kama Yohana alivyoandika katika waraka wake;
1 Yohana 4:20-21
20 Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.
21 Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.
Namalizia hivi;
-Mpende jirani yako kama nafsi yako
-Mpende adui yako
-Upendo wa Mungu na utawale kwetu.
Ibada njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
