VIDEOS

Angalia picha mjongeo (Video) za ibada na matukio maalum ya Usharika hapa https://m.youtube.com/@AZANIAFRONTCATHEDRAL

Date
Reading
Waamuzi 2:11-18

Jumatano asubuhi tarehe 23.09.2026;

Waamuzi 2:11-18

11 Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.

12 Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.

13 Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.

14 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao.

15 Kila walikokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.

16 Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara.

17 Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo.

18 Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.

Mungu amejaa huruma;
Baada ya Yoshua kufa, wana wa Israeli walielekea kwenye nchi yao kama walivyopewa. Ni baada ya hapo walifanya yaliyo maovu mbele za Mungu, wakawatumikia Mabaali. Walimuacha Mungu aliyewatoa Misri wakaifuata miungu mingine. Hasira ya Bwana iliwaka juu yao wakatekwa nyara na kuwekwa mikononi mwa adui zao. 

Kila walipokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kisha Bwana akawainulia  Waamuzi waliowaokoa na mikono ya watu waliowateka nyara. Lakini bado hawakuwasikiliza hao waamuzi, bado waliendelea na uovu! Bwana aliendelea kuwa nao akawainulia mwamuzi mwingine, ambaye aliwaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo, lakini bado naye hawakumsikiliza. Hasira ya Bwana ikawaka juu yao. 

Ukiendelea kusoma unaona Bwana akisema asingewafukuza katika Kanaani wale mataifa walioachwa na Yoshua, ili awajaribu Israeli kama wangeishika njia ya Bwana;

Waamuzi 2:20-23

20 Basi hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu;

21 mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa;

22 ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya Bwana kwenda katika njia hiyo, au sivyo.

23 Basi Bwana akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Pamoja na Israeli kumkosea Mungu bado hakuwaacha, aliwapa nafasi ya kumrudia. Kwa njia hii alionesha huruma yake kwao. Hata leo kwa huruma yake hutuita kutubu dhambi zetu na kumrudia wakati wote. Mungu wa huruma anakuita kutubu dhambi zako na kumtegemea yeye pekee katika maisha yako yote, kwani anayo ahadi ya kutupa uzima wa milele. Amina

Siku njema

Heri Buberwa 

I