
Ijumaa asubuhi tarehe 25.09.2026;
Marko 5:25-34
25 Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili,
26 na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya
27 aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake;
28 maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona.
29 Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule.
30 Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu?
31 Wanafunzi wake wakamwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, nawe wasema, Ni nani aliyenigusa?
32 Akatazama pande zote ili amwone yule aliyelitenda neno hilo.
33 Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote.
34 Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.
Mungu amejaa huruma;
Jana asubuhi tuliona Mkuu wa Sinagogi aliyeitwa Yairo akimuomba Yesu aende kumponya binti yake. Baada ya kuondoka na Yairo, akakutana na mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Huyu aligusa pindo la Yesu kwa imani na damu ikakauka. Yesu akamtangazia kwamba imani yake imemponya. Ndipo akaingia nyumbani kwa Yairo na kumfufua binti yake.
Tunaendelea kuiona huruma ya Yesu kwa kumponya binti Yairo, na mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Ni kwa huruma hiyo alikufa kwa ajili yetu ili tuokolewe toka dhambini. Tuzidi kukaa katika Kristo Yesu mwenye huruma maana ndiye mwenye hatma yetu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
