
Jumatatu asubuhi tarehe 14.09.2026
Kutoka 3:7-10
7 Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;
8 nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.
9 Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.
10 Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.
Mungu hujishughulisha na mambo yetu;
Bwana anamtokea Musa na kumwambia kwamba ameyaona mateso ya watu wake walioko Misri, amesikia kilio chao. Bwana anaendelea kusema kuwa ameshuka ili awaokoe watu wake kutoka kwenye mikono ya Wamisri, maana kilio chao kimemfikia na kuyaona mateso ambayo wanateswa na Wamisri.
Ni ujumbe ambao Bwana alinena na Musa akimwambia kuwa alikuwa anamtuma kwenda kuwatoa utumwani watu wake na kuwapeleka katika nchi aliyowaahidi baba zao. Kwa tafakari ya wiki hii, tunaweza kusema kuwa Mungu alikuwa anajishughulisha na mambo ya wana wa Israeli. Hata sasa Mungu hujishughulisha na mambo yetu, wajibu wetu ni kumwamini na kumtegemea katika yote. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa
