
Ijumaa asubuhi 11.09.2026;
Kutoka 10:24-26
24 Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie Bwana; kondoo zenu na ng'ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi.
25 Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia Bwana Mungu wetu dhabihu.
26 Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia Bwana, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia Bwana.
Tutende wajibu wetu kwa Mungu kwa uaminifu;
Ilikuwa ni baada ya balaa la tisa (giza) ndipo tunasoma Farao akimwambia Musa aondoke na watu wake kumtumikia Bwana wao, lakini waache kondoo na ng'ombe wao! Musa hakuwa tayari kuondoka bila mifugo yao, maana wasingepata sadaka ya kumtolea Bwana, alisisitiza kuondoka na mifugo/wanyama wao ili wakamtumikie Bwana kwa ukamilifu na sadaka za kuteketezwa.
Musa hakuangalia kuondoka tu na wana Israeli, bali aliangalia kuondoka bila kuacha kitu nyuma. Msisitizo wake ulikuwa kuondoka na wanyama wao kwa ajili ya sadaka (soma tena mstari wa 25). Pamoja na mambo mengine, Musa anazingatia kumtolea Mungu sadaka katika safari yao. Tuzingatie kumtolea Bwana mali alizotupa kwa kazi yake, huo ndiyo uwakili mwema mbele za Mungu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
