Jumamosi asubuhi tarehe 08.08.2026;
2 Petro 1:3-11
3 Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.
4 Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.
5 Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa,
6 na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa,
7 na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.
8 Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.
11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Mwenendo wenu uwe na hekima
Petro katika somo asubuhi ya leo anaandika juu ya wito na uteuzi wa Mkristo. Anasema kwa Mkristo aliyeitwa, Mungu amemkirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa kwa kumjua yeye Bwana. Anaendelea kuandika kwamba ahadi za Mungu ni kubwa, akiwahisi waaminio kuwa wema, kutumia maarifa, upendo na utume wa pamoja. Petro anasema pasipo maisha ya namna hiyo ni upofu, maana ni sawa na kusahau kutakaswa dhambi za zamani!
Petro asubuhi ya leo anatukumbusha kuuishi wito wetu kama tulivyoitwa. Yaani tunaalikwa kutenda yale yatupasayo kama kundi la wanaomwamini Yesu Kristo. Kila mmoja akitimiza wajibu wake, Kanisa la Mungu litakuwa imara na wote tutaimarika maana sisi sote ni mwili wa Kristo. Timiza wajibu wako hapo ulipo kuanzia nyumbani mwako, kazini na Kanisani. Uadilifu wako ndiyo utimilifu wa wito wako kama Mkristo. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
