Jumatano asubuhi 15.07.2026;
1 Yohana 3:17-20
17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?
18 Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli.
19 Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake,
20 ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote.
Upendo wa Mungu na utawale;
Utangulizi;
Yohana anatumia sehemu kubwa ya waraka akiwatia moyo wakristo katika safari ya imani. Anawahimiza moyo na kuwahimiza kutembea nuruni maana Mungu ni nuru, wakizitii amri zake (1Yoh 1:1-2:6). Yohana anaongelea "amri mpya, ya zamani", kupendana, kutoipenda dunia, kutosumbuliwa na "wapinga Kristo" wale wamkataao Yesu kama Kristo na Mwokozi (1Yoh 2:7-29)
Katika sura ya 3, Yohana anatofautisha wenye haki na waovu. Wenye haki huweka tumaini lao kwa Bwana, hujilinda na dhambi wakipendana. Waovu hutenda dhambi, huvunja sheria, wamejaa chuki. Binafsi nauona uhusiano wa moja kwa moja kati ya 1Yoh 3:16 na Yoh 3:16, hebu soma kwanza;
1 Yohana 3:16
[16]Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.
Yohana 3:16
[16]Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Ninachokiona kwenye mistari hii ni kwamba kifo cha Bwana Yesu ni maelezo ya upendo, na katika hili tunaitwa kujitoa kwa ajili ya wengine, yaani kujawa na upendo.
Somo lenyewe;
Mwanzoni Yohana waraka wake unaenda kiujumla zaidi, lakini inapofika mstari wa 17 unakuwa mahususi (specific). Anaakisi moja kwa moja kwa njia ya swali, kwamba mtu aliyejaliwa uwezo akamzuilia huruma mhitaji, upendo wa Mungu ukoje kwake? Yaani ukimuona mhitaji ukamuacha wakati unayo nafasi ya kumsaidia, upendo wa Mungu unasomekaje kwako?
Yohana hataki upendo liwe jambo la kufikirika, bali litafsiriwe kwa vitendo. Yohana aanatumia picha ya mwenye nacho na asiye nacho kuonesha uhusiano unaotakiwa miongoni mwa waaminio. Inapotokea mmmoja anao uwezo, basi huja wajibu kama Mtume Paulo anavyoandika;
1 Timotheo 6:17-19
[17]Walio matajiri wa ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.
[18]Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane na wengine kwa moyo;
[19]huku wakijiwekea akiba iwe msingi mzuri kwa wakati ujao, ili wapate uzima ulio kweli kweli.
Tuendelee;
Ukisoma nyuma kidogo, Yohana anasema tupendane;
1 Yohana 3:11
[11]Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi;
Amri ya kupendana imerudiwa sana katika Agano jipya. Inatokea mara 55 kama amri ya moja kwa moja. Hapa ni mifano michache;
Mathayo 5:44
[44]lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
Mathayo 22:39
[39]Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.
Yohana 13:34
[34]Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.
1 Wakorintho 16:14
[14]Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo.
Wagalatia 5:13
[13]Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.
Hivyo, jambo la muhimu hapa ni kumpenda Mungu kwa hali zote, na kuwapenda jirani zetu kama nafsi zetu. Tuuchukue mfano wa Kristo alivyotupenda sisi, tukiwapenda wenzetu.
Mkazo wa somo la leo ni "kutafsiri upendo kwa vitendo" na siyo kwa maneno. Upendo wa Yesu aliuonesha kwa tendo la kufa msalabani (16) na hata somo la leo linauliza juu ya tendo la aliye nacho kutomjali asiye nacho.
Mungu anatuita kujitoa, kusaidia, kwa Imani mara tuonapo wenzetu wana uhitaji. Uaminifu katika dogo hutufanya tuaminike zaidi. Vivyo tukiwasaidia wenzetu, Mungu hutubariki zaidi, hivyo kutupa zaidi. Tunapowasaidia wengine tunatafuta kuonja uzuri wa Bwana hatua kwa hatua, pale anapotupa baraka.
Baadhi yetu hufikiri kuwa mtu huwezi kumsaidia kila mwenye uhitaji. Inawezekana ni kweli, lakini kwa nilivyosoma mstari wa 17, nafikiri hivi;
"Mungu hategemei wewe umsaidie kila mtu duniani, lakini anategemea uwasaidie wale aletao kwako ukitumia rasilimali alizokupa" (soma tena)
-Kumbuka mfano wa msamaria aliyemsaidia majeruhi, aliyemuona akipita.
-Yesu hakuponya kila kilema katika Galilaya
-Yesu hakuponya kila kipofu
-Vile vile, Mitume hawakuwaondolea watu umaskini au kuwafanya vilema watembee. Bali waliomba neema na upendo wa Mungu juu ya wahitaji waliowajia. Waliwapa pesa wale waliojua wana uhitaji. Waliwasaidia wale Mungu aliowaleta kwao kwa kutumia rasilimali walizopewa kama sala, uponyaji, fedha, ardhi, na hata maisha yao. Narudia;
"Mungu hategemei wewe umsaidie kila mtu duniani, lakini anategemea uwasaidie wale aletao kwako ukitumia rasilimali alizokupa"
Mwisho;
Tunaposhindwa kuwa msaada kwa ndugu zetu, Mungu anaona upendo haumo ndani yetu. Hapa ni muhimu kutafakari kama tunao upendo mioyoni mwetu. Historia ya wokovu ni simulizi ya upendo, kwa jinsi Yesu alivyokufa msalabani. Upendo huu inabidi udhihirike kwetu kama kweli sisi ni wanafunzi wake. Upendo ni gharama, maana huusisha kujitoa kwanza, halafu kutoa tulivyo navyo.
Tunaitwa kutafsiri na kuonesha upendo kwa vitendo. Huo ndiyo upendo unaogusa Taifa la Mungu. Gusa mahitaji ya wengine kwa uhalisia, kama Yesu alivyojitoa kwa uhalisia. Usipofanya hivyo upendo haumo ndani yako!
Nukuu ya leo;
"Mungu hategemei wewe umsaidie kila mtu duniani, lakini anategemea uwasaidie wale aletao kwako ukitumia rasilimali alizokupa"
Uwe na siku njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
