Jumatatu asubuhi tarehe 27.07.2026
1 Samweli 12:20-25
20 Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote.
21 Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili,
22 visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza Bwana kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe.
23 Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka
24 Mcheni Bwana tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu.
25 Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.
Mungu hupendezwa na moyo wa toba;
Ni sehemu ya hotuba ya Samweli ambaye sasa ni Mzee akiwaaga Israeli. Tunaona akiwaambia kuwa pamoja na kutenda dhambi kwao wasiache kumfuata Bwana, bali wamtumikie kwa moyo wote. Anawataka wasifuate vitu vya ubatili visivyoweza kuwasaidia wala kuwaokoa, maana Bwana mwenyewe hatawaacha.
Samweli anamalizia akiwasisitizia kumcha Bwana tu na kumtumikia wakikumbuka alivyowatendea mambo makuu. Anawapa angalizo, kwamba wakiendelea kutenda mabaya wataangamia wote. Ni ujumbe unaotutaka kutoiacha imani katika Yesu Kristo, kuishi maisha ya toba na kumtumikia Mungu wa kweli. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa
